Klabu ya Singida BS imethibitisha kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani Jonathan Sowah akitokea klabu ya Simba.
Taarifa iliyotolewa na Singida BS, imebainisha kuwa Sowah amerejea tena kunako klabu hiyo baada ya kipindi kifupi cha kuwatumikia Wekundu wa Msimbazi.
Nyota huyo raia wa Ghana amesaini mkataba wa miaka mitatu utakaomuweka Singida hadi mwaka 2029.
Mshambuliaji huyo 'mtukutu' ameondoka Simba huku akikabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu.
Simba ilimfungia kwa muda mrefu na baadae walipomfungulia aligomea kwenda kufanya mazoezi na kikosi cha timu ya vijana U20.
Ni rasmi sasa amerejea kwa waajiri wake wa zamani ambao aliwatumikia msimu wa 2024/25 akitua kwenye usajili wa dirisha dogo na kufanikiwa kufunga mabao 14.