Kocha wa zamani wa Azam FC, Youssoupha Dabo, ameteuliwa rasmi kuwa kocha mkuu mpya wa Timu ya Taifa ya Libya kwa mkataba wa mwaka mmoja. Shirikisho la Soka la Libya limethibitisha uteuzi huo, likimkabidhi jukumu la kuiongoza timu hiyo kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.
Dabo anachukua mikoba hiyo akiwa tayari anaifahamu vyema timu ya taifa ya Libya, baada ya kuwahi kuwa kocha msaidizi chini ya Aliou Cissé. Kabla ya uteuzi huo, kocha huyo raia wa Senegal amepata uzoefu mkubwa barani Afrika kupitia vilabu vya Teungueth FC, ASC Jaraaf, Azam FC ya Tanzania na AS Vita Club ya DR Congo, sambamba na kuinoa timu ya taifa ya Senegal chini ya umri wa miaka 20.
Jukumu kubwa la Dabo sasa litakuwa kuijenga upya Libya na kuiongoza katika harakati za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. Uongozi wa Shirikisho la Soka la Libya unaamini uzoefu wake katika ngazi ya klabu na timu za taifa utasaidia kuirejesha timu hiyo katika ushindani wa soka la Afrika.