Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limetangaza kuwa fainali ya Kombe la Dunia 2026 itakuwa na onesho rasmi la burudani wakati wa mapumziko, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo kuanzisha utaratibu huo.
Kwa mujibu wa FIFA, onesho hilo litafanyika wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza na linatarajiwa kudumu kwa takribani dakika 11.
Kutokana na hilo, muda wa mapumziko utaongezwa kutoka dakika 15 za kawaida hadi kati ya dakika 20 na 25 ili kuruhusu maandalizi na kuondolewa kwa jukwaa la burudani bila kuathiri ratiba ya mchezo.
Fainali hiyo imepangwa kuchezwa Julai 19, 2026, katika Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani, na itakuwa ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kuwa na onesho rasmi la burudani wakati wa mapumziko, kwa mfumo unaofanana na Super Bowl ya NFL.