Klabu ya Singida Black Stars imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo mshambuliaji Marcel Canadi (28) raia wa Austria, katika hatua ya kuendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kusaini mkataba wa muda mfupi wa miezi sita, huku nyota huyo akitarajiwa kujiunga na kikosi hicho mara baada ya kukamilika kwa taratibu za mwisho za usajili.
Canadi si jina geni katika soka la Ulaya, kwani aliwahi kuitumikia Borussia Mönchengladbach II ya Ujerumani, ambako alipata uzoefu mkubwa kabla ya kuendelea na safari yake katika vilabu mbalimbali barani humo.
Uongozi wa Singida Black Stars unaamini kuwa uwezo wa Canadi wa kucheza nafasi mbalimbali za ushambuliaji utaongeza ushindani ndani ya kikosi na kukipa nguvu zaidi kuelekea msimu wa 2026/27.
Iwapo kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa, Marcel Canadi atakuwa mmoja wa nyota wapya watakaovaa jezi ya Singida Black Stars, huku mashabiki wakisubiri kuona mchango wake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.