Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limemtangaza rasmi mwamuzi kutoka Slovenia, Slavko Vini, kuwa msimamizi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2026 utakaowakutanisha Hispania na Argentina. Fainali hiyo itachezwa Jumapili, Julai 19, 2026, katika Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani, kuanzia saa 4:00 usiku.
Vini, mwenye umri wa miaka 46, ni mwamuzi wa kimataifa wa FIFA tangu mwaka 2010 na anatajwa kuwa miongoni mwa waamuzi wenye uzoefu mkubwa katika soka la kimataifa. Katika kipindi chake cha uamuzi, amechezesha mechi nyingi za hadhi ya juu katika mashindano ya FIFA na UEFA.
Miongoni mwa mechi kubwa alizowahi kusimamia ni fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2024 kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund, pamoja na michezo ya Kombe la Dunia la Klabu 2025 lililofanyika nchini Marekani. Uzoefu huo umechangia FIFA kumpa jukumu la kusimamia fainali ya mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.
Uteuzi wa Vini unakuja huku dunia ikisubiri kwa hamu pambano la fainali kati ya Hispania na Argentina, ambapo mataifa hayo mawili yatapambana kuwania taji la Kombe la Dunia 2026 katika mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia za mamilioni ya mashabiki duniani.