Klabu ya Simba SC imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kujenga kikosi imara kuelekea msimu mpya baada ya kukamilisha hatua za mwisho za kuwasajili nyota wawili, Keletso Makgalwa na Ibrahim Doumbia.
Mshambuliaji Ibrahim Doumbia, mwenye umri wa miaka 22 kutoka Mali, tayari amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Wekundu wa Msimbazi. Nyota huyo anajiunga na Simba kama mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na AS Korofina ya Mali.
Taarifa zinaeleza kuwa Doumbia amepewa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine endapo ataonyesha kiwango cha kuridhisha ndani ya kikosi cha Simba.
Straika huyo anakuja akiwa na rekodi bora kutoka Ligi Kuu ya Mali, ambapo msimu uliopita aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17 katika michezo 24. Mbali na mabao hayo, alitoa pasi nne za mabao na pia alifunga mabao manne katika michuano ya Kombe la FA, akimaliza nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji.

Iwapo taratibu zote zitakamilika kwa wakati, Doumbia anatarajiwa kuonekana kwa mara ya kwanza akiwa na jezi ya Simba katika michuano ya CECAFA Kagame Cup inayotarajiwa kuanza Julai 24 nchini Rwanda.
Wakati huohuo, kiungo mshambuliaji wa pembeni kutoka Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, amewasili jijini Dar es Salaam mapema leo kwa ajili ya kukamilisha usajili wake.

Makgalwa mwenye umri wa miaka 29, ambaye alikuwa akiichezea Sekhukhune United ya Afrika Kusini, amewasili nchini akiwa ameongozana na wakala wake, hatua inayoashiria kuwa utambulisho wake rasmi ndani ya Simba umesalia kuwa suala la muda.
Inaelezwa kuwa usajili wa Makgalwa umefanikishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushawishi wa kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, ambaye anaamini winga huyo ataleta ubunifu, kasi na uzoefu mkubwa katika safu ya ushambuliaji.