Klabu ya Singida Black Stars inatajwa kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua, raia wa Ivory Coast, katika moja ya usajili mkubwa unaovuta hisia kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Ahoua, ambaye aliwahi kung'ara akiwa na Simba SC kwa kiwango chake bora cha kutengeneza na kufunga mabao, anarejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuachana na klabu ya CR Belouizdad ya Algeria.
Nyota huyo amesitisha mkataba wake na Belouizdad kwa makubaliano ya pande zote, hatua iliyomfanya kuwa mchezaji huru kabla ya kutua Singida Black Stars.
Iwapo usajili huo utathibitishwa rasmi, utakuwa ni nyongeza kubwa kwa Singida Black Stars ambao wanaendelea kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Ahoua anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Singida Black Stars kitakachoshiriki michuano ya CECAFA Kagame Cup, inayotarajiwa kuanza Ijumaa, Julai 24. Uwepo wake kwenye kikosi hicho unatarajiwa kuongeza ubora mkubwa katika eneo la kiungo cha ushambuliaji kutokana na uzoefu wake na uwezo wake wa kubadili matokeo ya mchezo.
Nyota huyo anarejea Tanzania akiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kumaliza msimu wa 2024/25 kama mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC. Sasa anatarajiwa kuendeleza makali yake, lakini safari hii akiwa amevaa jezi ya Singida Black Stars.