Klabu ya Singida Black Stars imeendelea kujiimarisha kuelekea msimu mpya baada ya kumrejesha beki wa kati wa timu ya taifa ya Nigeria, Benjamin Tanimu, kwa mkataba wa miaka miwili.
Tanimu, mwenye umri wa miaka 23, anarejea Singida Black Stars akitokea klabu ya Maghreb Fès ya Morocco, ambako alicheza baada ya kuondoka Tanzania. Taarifa zinaeleza kuwa mkataba wake mpya na Singida ni wa miaka miwili, huku ada ya usajili ikibaki kuwa siri.
Anatarajiwa kujiunga na kikosi hicho katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya nchini Rwanda.
Beki huyo tayari anaifahamu vizuri mazingira ya soka la Tanzania. Kabla ya kujiunga na Maghreb Fès, aliwahi kuzichezea Ihefu FC na baadaye Singida Black Stars, ambapo alionyesha kiwango bora kilichomfungulia milango ya kucheza nje ya nchi.
Kabla ya safari yake ya kimataifa, Tanimu aliichezea Bendel Insurance ya Nigeria, ambako aliibuka kuwa mmoja wa mabeki bora katika Ligi Kuu ya Nigeria. Umhiri wake ulimpa nafasi ya kuitwa katika kikosi cha Super Eagles, timu ya taifa ya Nigeria.
Mbali na kucheza Morocco, Tanimu pia aliwahi kuhusishwa na klabu ya Crawley Town ya England, jambo lililoonyesha jinsi kiwango chake kilivyokuwa kikifuatiliwa na timu mbalimbali.
Kurejea kwake Singida Black Stars kunatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa klabu hiyo wa kujenga kikosi imara kitakachoshindana katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine ya msimu wa 2026/27.