Klabu ya Inter Miami imeendelea kuvutia macho ya dunia ya soka baada ya kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji wa Brazil, Casemiro, ambaye sasa ataungana na nyota wa Argentina, Lionel Messi, katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Casemiro ametua Inter Miami kama mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Manchester United, ambako alitumia misimu kadhaa akicheza soka la kiwango cha juu England. Usajili huo unampa nafasi ya kuendelea na changamoto mpya akiwa sambamba na baadhi ya mastaa wakubwa duniani.
Kujiunga kwa kiungo huyo mwenye uzoefu mkubwa kunatarajiwa kuongeza uimara katika eneo la katikati ya uwanja la Inter Miami. Casemiro anajulikana kwa uwezo wake wa kukaba, kushinda mipira, kuongoza mchezo na uzoefu alioupata akiwa na klabu kubwa kama Real Madrid na Manchester United.
Reunion ya Mastaa wa Dunia
Casemiro na Messi wamekuwa wapinzani wakubwa kwa miaka mingi wakati wa kipindi ambacho Mbrazili huyo akiichezea Real Madrid na Messi akiwa Barcelona katika mechi za El Clásico. Sasa wawili hao watakuwa upande mmoja wakitumikia Inter Miami katika harakati za kuipa klabu hiyo mafanikio zaidi.
Inter Miami imekuwa ikijenga kikosi chenye majina makubwa katika soka la dunia, huku ujio wa Messi ukibadili hadhi ya klabu hiyo kimataifa. Kuongezwa kwa Casemiro kunaongeza uzoefu mwingine wa kiwango cha juu ndani ya timu hiyo.
Katika maisha yake ya soka, Casemiro amejijengea jina kama mmoja wa viungo bora wa kizazi chake. Akiwa Real Madrid alifanikiwa kushinda mataji makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya mara kadhaa kabla ya kuhamia Manchester United.
Hata hivyo, usajili huo umeibua uchunguzi kutoka kwa MLS kuhusu mchakato wa uhamisho huo, huku ligi hiyo ikifuatilia suala la haki za usajili (discovery rights) zinazohusishwa na klabu nyingine.