Klabu ya Barcelona imemtambulisha rasmi mshambuliaji wa Ujerumani, Karim Adeyemi, kuwa mchezaji wake mpya baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Borussia Dortmund.
Adeyemi, mwenye umri wa miaka 24, amejiunga na miamba hiyo ya La Liga kwa mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Camp Nou hadi Juni 2031.
Barcelona imelipa euro milioni 22 kama ada ya msingi ya usajili, huku makubaliano yakijumuisha nyongeza (bonasi) zinazoweza kufikisha euro milioni 7 kulingana na mafanikio ya mchezaji na klabu.
Kocha Hansi Flick alihusika kwa kiasi kikubwa katika kushinikiza usajili huo kutokana na kumfahamu Adeyemi tangu walipokuwa pamoja katika timu ya taifa ya Ujerumani. Flick anavutiwa na kasi, uwezo wa kucheza pande zote za ushambuliaji na presha kubwa anayoweka kwa wapinzani anapopoteza mpira.Β
Adeyemi anatarajiwa kuongeza ushindani kwenye safu ya ushambuliaji ya Barcelona, akitoa chaguo zaidi kwa kocha Flick pamoja na kuwapa mapumziko wachezaji wa pembeni pale itakapohitajika. Pia anaweza kutumika katika nafasi mbalimbali za mbele kutokana na uwezo wake wa kucheza kama winga wa kulia, kushoto au mshambuliaji wa kati.
Changamoto moja inayomkabili mara baada ya kuwasili ni uchaguzi wa namba ya jezi, kwani namba 27 aliyokuwa akiitumia Borussia Dortmund haiwezi kutumika kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza Barcelona kutokana na kanuni za La Liga.
Usajili wa Adeyemi ni sehemu ya mkakati wa Barcelona kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya, huku klabu ikiendelea kutafuta njia ya kujenga kikosi chenye ushindani mkubwa ndani na nje ya Hispania.