Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) limemtangaza rasmi Jurgen Klopp kuwa kocha mkuu mpya wa Timu ya Taifa ya Ujerumani kwa mkataba utakaodumu hadi baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2030.
Klopp, ambaye alijijengea heshima kubwa akiwa kocha wa Borussia Dortmund na baadaye Liverpool, anarejea benchi la ufundi baada ya kuachana na Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2023/24 na kufanya kazi kama Mkuu wa Soka wa kimataifa wa kampuni ya Red Bull.
Sasa amepewa jukumu la kuirejesha Ujerumani kwenye ubora wake baada ya kipindi kigumu katika mashindano makubwa ya kimataifa.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 anarithi mikoba ya Julian Nagelsmann, ambaye aliondoka kufuatia kampeni isiyoridhisha ya Ujerumani kwenye Kombe la Dunia la 2026. Klopp anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake katikati ya mwezi Agosti, huku mechi yake ya kwanza ikipangwa kuwa dhidi ya Uholanzi kwenye michuano ya UEFA Nations League mwezi Septemba.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Klopp alisema ni heshima kubwa kupewa nafasi ya kuiongoza timu ya taifa ya nchi yake, akieleza kuwa anaamini Ujerumani ina vipaji vya kutosha kurejea katika ushindani wa juu duniani.
Katika maisha yake ya ukocha, Klopp amewahi kuiongoza Mainz 05, Borussia Dortmund na Liverpool, ambako alitwaa mataji makubwa yakiwemo Ligi Kuu England, UEFA Champions League, FA Cup na Kombe la Dunia la Klabu. Mafanikio hayo yamemfanya kuwa mmoja wa makocha wenye heshima kubwa zaidi katika soka la dunia.