Rais wa Klabu ya Yanga SC, Injinia Hersi Said, amewatolea uvivu na kuwashukia vikali wadau wa soka wanaobeza usajili wa wachezaji wazawa uliofanywa na klabu hiyo, akitaja ukosoaji huo kama mtazamo hasi usio na tija kwa maendeleo ya soka la Kitanzania.
Akizungumza usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano maalumu wa klabu hiyo, Injinia Hersi amesema uongozi wa Yanga utakuwa wa "hovyo" kama utashindwa kuwapa fursa wachezaji wa ndani kuonyesha vipaji vyao kwenye timu kubwa.
"Mchezaji anayetoka timu nyingine ya hapa nyumbani, akija Yanga hata kwa msimu mmoja tu, kiwango chake hakiwezi kubaki pale pale. Thamani yake inaongezeka na kiwango kinakua kwa sababu ya mazingira na ushindani uliopo hapa," alisema Hersi kwa msisitizo.
Rais huyo aliongeza kuwa kelele na maneno ya kubeza usajili huo hayatawakatisha tamaa, na badala yake wataendelea kuwasajili na kuwakuza nyota wa ndani ili kulisaidia Taifa na timu ya taifa, Taifa Stars.
Katika dirisha hili la usajili kuelekea msimu mpya wa mashindano, Yanga imetambulisha rasmi wachezaji wazawa sita waliotua kwa mabingwa hao wa nchi.
Wachezaji hao ni:
- Hussein Mihambo (Mshambuliaji β kutoka Mashujaa FC)
- Juma Issa Abushiri (Winga β kutoka Fountain Gate)
- Abdulnasir Muhamed (Beki wa pembeni β kutoka Mashujaa FC)
- Mohamed Mussa (Beki wa kati β kutoka Mashujaa FC)
- Erick Mwijage (Winga β kutoka KMC)
- Suleiman Mbarouk "Mpemba D" (Kiungo β kutoka JKU ya Zanzibar)
Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa mchanganyiko wa wachezaji hao sita wa ndani na nyota wapya wa kigeni waliosajiliwa, unalenga kutengeneza kikosi kipana kitakachopambana kutetea mataji ya ndani na kufika mbali zaidi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).