Mchezo wa kwanza wa Kundi B katika michuano ya CECAFA Kagame Cup kati ya Simba SC na Mogadishu City FC umemalizika kwa sare ya bila kufungana, huku timu zote zikigawana pointi moja katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Simba SC chini ya kocha mkuu Steve Barker ilianza mchezo ikiwa na kikosi chenye mchanganyiko wa nyota wengi wapya waliosajiliwa katika dirisha hili la usajili. Wekundu wa Msimbazi walitawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini walikumbana na ukuta imara wa ulinzi wa Mogadishu City ambao ulikaa nyuma kwa muda mwingi kuhakikisha lango lao halifungwi.
Katika dakika 15 za mwisho, Simba iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya Barker kufanya mabadiliko ya kuwaingiza Clatous Chama, Shomari Kapombe, Anicet Our, Keletso Makgalwa, Ibrahim Doumbia na Jabeer ili kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Doumbia alikaribia kuandika bao la ushindi katika dakika za mwisho za mchezo, huku Makgalwa pia akitengeneza nafasi nyingine nzuri, lakini safu ya ulinzi ya Mogadishu City iliendelea kuwa imara na kuondoa hatari zote langoni mwao.
Baada ya matokeo ya michezo ya leo, Jamus FC inaongoza Kundi B ikiwa na pointi tatu baada ya kuifunga Singida Black Stars mabao 2-0 katika mchezo wa awali. Simba SC na Mogadishu City zinafuatia zikiwa na pointi moja kila moja.
Simba sasa itarejea uwanjani Jumanne, Julai 28, kukutana na Jamus FC katika mchezo unaotarajiwa kuwa na presha kubwa kwa Wekundu wa Msimbazi katika harakati za kuwania nafasi ya kufuzu hatua inayofuata.