Kiungo mshambuliaji wa Simba Keletso Makgalwa juzi alianza kutema cheche zake katika mchezo wake wa kwanza michuano ya kombe la Kagame dhidi ya Mogadishu City ambao ulimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Akitambulishwa saa chache kuelekea mchezo huo, kocha mkuu wa Simba Steve Barker alimpa nafasi kwenye dakika 15 za mwisho kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mastaa wengine wapya kama Ibrahim Doumbia na Jabeer.
Kuingia kwake na wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza ambao walianzia nje kwenye mchezo huo, kulibadili kabisa taswira ya mchezo wengi wakiamini kama Barker angewaanzisha pengine Mogadishu City wangeondoka na kapu la mabao.

Akizungumza baada ya mchezo huo Keletso alisema ametua Msimbazi kwa kazi moja tu, kuisaidia timu iweze kushinda mechi, kutwaa mataji na kuhakikisha wanatimiza malengo ya klabu
“Nimekuja Simba kufanya kazi, kupambana kwa ajili ya timu na kushinda mataji. Nitajitolea kwa kila kitu kuhakikisha mashabiki wanafurahia kile nitakachokitoa uwanjani. Subirini muone,” alisema Makgalwa kwa kifupi.
Kiungo huyo fundi ametua Msimbazi akitokea klabu ya Sekhukhune United akiwa ni pendekezo la kocha Steve Barker.
Alikuwa tegemeo kwenye kikosi cha Sekhukhune kutokana na mchango wake mkubwa kwenye mabao ya timu hiyo.
Baada ya kumshuhudia kwa dakika chache, Wanasimba sasa wana matarajio makubwa kwake wakiamini anakwenda kuongeza ubunifu eneo la ushambuliaji na kutengeneza nafasi nyingi za mabao.