Hatma ya kiungo mshambuliaji Neo Maema ndani ya Simba SC inaendelea kubaki njia panda baada ya mazungumzo ya kumuongeza mkataba kushindwa kuzaa matunda hadi sasa.
Baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika, uongozi wa Simba ulikuwa na matumaini ya kuendelea kuwa na huduma ya nyota huyo raia wa Afrika Kusini. Hata hivyo, mipango hiyo imekutana na kikwazo kikubwa kufuatia Mamelodi Sundowns kutumia kipengele cha kuongeza miaka miwili kwenye mkataba wa mchezaji huyo.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa kocha wa Simba, Steve Barker, bado anamuhitaji Maema kama sehemu muhimu ya kikosi chake kwa msimu ujao. Kocha huyo anaamini uwezo na uzoefu wa kiungo huyo unaweza kuisaidia Simba katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Kutokana na hatua ya Sundowns, Simba italazimika kuingia kwenye mazungumzo mapya na mabingwa hao wa Afrika Kusini endapo itahitaji kuendelea kuwa na Maema. Hata hivyo, mshahara anaouhitaji mchezaji huyo umeonekana kuwa kikwazo kikubwa katika kufikia makubaliano.
Maema ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa ndani ya kikosi cha Simba, hali inayoufanya uongozi wa klabu hiyo kutathmini kwa makini kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wake.
Kwa sasa, kiungo huyo yupo nchini Afrika Kusini, wakati Simba ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya kupitia michuano ya CECAFA Kagame Cup inayofanyika Kigali, Rwanda.
Wakati huo huo, Simba tayari imeimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili kiungo mshambuliaji Ibrahim Jabeer kutoka Stellenbosch FC. Ujio wa Jabeer unaonekana kupunguza presha ya kuhakikisha Maema anabaki Msimbazi, hasa kutokana na gharama kubwa zinazohitajika kukamilisha dili hilo.
Jabeer ana uwezo wa kucheza katika nafasi na majukumu yaliyokuwa yakifanywa na Maema, ingawa Barker bado anatamani kuwa na wachezaji hao wote wawili ndani ya kikosi chake ili kuongeza ushindani na ubora kuelekea msimu mpya.