Ndoto ya Besiktas ya kumsajili nyota wa Misri Mohamed Salah imeingia kwenye wakati mgumu baada ya mazungumzo kati ya pande hizo kufikia hatua ya kusimama kutokana na tofauti za kifedha.
Besiktas ilikuwa imeonyesha nia kubwa ya kumpata Salah baada ya kuachana na Liverpool, huku klabu hiyo ya Uturuki ikiamini kuwa uzoefu na ubora wa mshambuliaji huyo ungeongeza nguvu kubwa kwenye kikosi chao.
Hata hivyo, dili hilo limeanza kuwa gumu baada ya kushindwa kufikia makubaliano kuhusu masuala ya fedha.
Mkurugenzi wa michezo wa Besiktas, Önder Özen, amethibitisha kuwa mazungumzo yalifanyika na yalikuwa yameenda vizuri katika hatua za awali, lakini changamoto zilianza kujitokeza walipoingia kwenye sehemu ya masuala ya kifedha.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, madai yanayohusisha maslahi binafsi, haki za picha (image rights) na gharama nyingine za dili yamekuwa sehemu ya vikwazo vilivyoifanya Besiktas kusitisha kwa muda mchakato huo.
"Tulimpa ofa Salah, lakini wawakilishi wake waliwasilisha mahitaji ya kifedha yaliyofanya mazungumzo kuwa magumu. Tuna mipaka yetu ya usajili na hatuwezi kuvuka kiwango tulichojiwekea," alisema Özen.
Awali kulikuwa na taarifa zilizodai kuwa Salah alikuwa karibu kujiunga na Besiktas, lakini wakala wake Ramy Abbas aliwahi kukanusha kuwa hakuna makubaliano yaliyokamilika kuhusu hatma ya mteja wake.
Kwa sasa, Besiktas bado haijafunga rasmi mlango wa usajili huo, lakini imeweka wazi kuwa haitatoa ofa nyingine inayozidi mipaka yake ya kifedha. Klabu hiyo inasubiri kama upande wa Salah utakuwa tayari kukubali masharti yaliyowekwa.
Salah, ambaye ameacha alama kubwa katika soka la dunia baada ya miaka kadhaa ya mafanikio akiwa Liverpool, bado anavutia vilabu mbalimbali kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao, uzoefu wa mashindano makubwa na thamani yake kibiashara.