Ligi Kuu ya NBC imeendelea leo zikishuhudiwa mechi mbili za kukata na shoka kwa timu za Azam FC na Mbeya City kuondoka na alama tatu muhimu.
Katika mchezo uliopigwa kwenye Dimba la Azam Complex, Chamazi, wenyeji Azam FC walifanikiwa kuichapa Pamba Jiji mabao 2-1.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulitawaliwa na ufundi mwingi, ambapo magoli ya Azam FC yalipachikwa wavuni na nyota wao Enoch Malia na Abdul Sopu.
Pamba Jiji walijitahidi kupambana na kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Nonyem Okorocha, lakini halikutosha kuwazuia matajiri hao wa viunga vya Chamazi kuondoka na ushindi.
Wakati huohuo, jijini Mbeya ulipigwa mchezo wa mapema ambapo wenyeji Mbeya City wamezinduka na kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Sokoine.
Mashujaa FC ndio waliokuwa wa kwanza kuziona nyavu za Mbeya City kupitia goli lililofungwa na Hijja Shamte, goli lilioamsha ari ya wenyeji.
Hata hivyo, Mbeya City walionyesha ukomavu kwa kufanya mapinduzi makubwa (comeback) kipindi cha pili na kusawazisha makosa kupitia mabao ya Adily Buha na Oscar Mwajanga, na hivyo kuwapa mashabiki wa Mbeya burudani na pointi zote tatu nyumbani.



