Nyota wa zamani wa Manchester City na Barcelona, Yaya Touré, ameandika historia baada ya kuifikisha Slovan Bratislava UEFA Champions League, akiwa kocha mkuu wa kwanza Mwafrika kufanikisha hatua hiyo.
Touré, mwenye umri wa miaka 43, amefanikisha hilo baada ya Slovan Bratislava kufuzu katika mchezo wa mchujo uliomalizika kwa mikwaju ya penalti, kufuatia bao la Cristian Martínez lililofungwa katika dakika ya 100.
Touré aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Slovan Bratislava mwezi Juni mwaka huu na kusaini mkataba wa miaka mitatu. Nafasi hiyo imekuwa kazi yake ya kwanza kama kocha mkuu, baada ya awali kufanya kazi kama kocha msaidizi katika klabu na timu mbalimbali, ikiwemo timu ya taifa ya Saudi Arabia.
Tangu alipokabidhiwa jukumu hilo, Touré ameendelea kuwa na mwanzo mzuri wa kazi yake ya ukocha, akiwa bado hajapoteza mchezo tangu kuanza kuinoa Slovan Bratislava. Mafanikio hayo yanaongeza historia katika safari yake mpya ya ukocha baada ya kuwa miongoni mwa viungo bora barani Ulaya akiwa mchezaji.



