Simba SC imeendeleza rekodi yake ya ushindi kwa asilimia 100 msimu huu baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam.
Ulikuwa mchezo ambao Simba ilitawala kwa muda mwingi, huku Wekundu wa Msimbazi wakimiliki mchezo na kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga ukilinganisha na wapinzani wao.
Katika kipindi cha kwanza, washambuliaji wa Simba walikosa umakini katika umaliziaji na kushindwa kutumia nafasi kadhaa za wazi walizozipata. Kwa upande wao, Coastal Union waliweka mkazo zaidi katika kujilinda na kuzuia mashambulizi ya Simba.
Baada ya mfululizo wa mashambulizi kwenye lango la Coastal Union, Simba hatimaye ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 74 kupitia Ismail Touré, aliyemalizia kwa kichwa krosi nzuri ya Anicet Oura.
Katika dakika za lala salama, Simba ilipata mkwaju wa penalti baada ya Elie Mpanzu kuonekana kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, baada ya tukio hilo kufanyiwa mapitio kupitia mfumo wa FVS, uamuzi wa kutoa penalti ulifutwa.
Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa Simba kuandikisha ushindi wake wa nne mfululizo msimu huu, huku ikirejea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 12.
Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea na mwanzo bora wa msimu, ikiwa bado haijapoteza mchezo wala kupoteza alama katika michezo yake minne ya kwanza.



