Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold, licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na changamoto za majeraha.
Simba kesho Jumatatu itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwa na dhamira ya kuibuka na ushindi mbele ya Geita Gold na kujihakikishia alama tatu muhimu.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari leo kuelekea mchezo huo, Barker amesema wamefanya maandalizi mazuri kwa wachezaji waliopo na anaamini wana nafasi kubwa ya kupata ushindi.
“Tumefanya maandalizi mazuri kwa wachezaji waliopo na tuko tayari kwa mchezo dhidi ya Geita Gold hapo kesho,” alisema Barker.
Kocha huyo amesema wanaifahamu vizuri Geita Gold na wanatarajia kupata upinzani mkubwa kutokana na ubora wa wachezaji na benchi la ufundi la wapinzani wao.
“Tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ngumu ambayo ina wachezaji bora mmoja mmoja na wana kocha mzuri pia,” aliongeza.
Barker amesema muda walioupata kwa ajili ya maandalizi umewasaidia kukiweka kikosi katika hali nzuri na sasa wanaamini wana uwezo wa kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani.
“Tumekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa na naamini tuna nafasi nzuri ya kupata alama tatu nyumbani hapo kesho,” alisema Barker.
Simba yaendelea kukabiliwa na majeraha
Katika mchezo huo, Simba itaendelea kuwakosa Yusuph Kagoma na Nickson Kibabage ambao bado wanasumbuliwa na majeraha.
Hata hivyo, kuna habari njema kwa upande wa kikosi hicho baada ya Ibrahim Jabaar kutarajiwa kurejea na kuwa sehemu ya mipango ya timu katika mchezo huo.
Nae kocha wa Geita Gold Zubri Katwila ametamba kuwa licha ya ubora pamoja na uzoefu wa wapinzani wao, wako tayari kukabiliana nao katika mchezo ambao utakuwa na upinzani mkali.
Geita Gold imeanza vyema msimu huu ikukusanya alama 7 katika mechi nne. Wameshinda mechi mbili, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.



