Malick Yalcouyé ameibuka kuwa miongoni mwa majina yaliyozungumziwa zaidi baada ya kufunga bao katika mchezo wa Brighton dhidi ya Chelsea, huku kiwango chake uwanjani kikifanya mashabiki wengi kuvutiwa na kipaji chake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo, akifunga bao moja, akipiga mashuti mawili yaliyolenga lango, kushinda asilimia 77.8 ya mipambano yake na kukamilisha asilimia 80 ya majaribio yake ya kuwapita wapinzani..jpg)
Baada ya muonekano wake kuibua mijadala mitandaoni na baadhi ya watu kuanza kuhoji umri wake, ASEC Mimosas ya Ivory Coast imeamua kuweka wazi historia yake. Klabu hiyo imechapisha picha za Yalcouyé tangu akiwa kwenye akademi yake akiwa mdogo, kwa lengo la kuthibitisha kuwa taarifa zinazohusu umri wake si za kweli. Yalcouyé pia ana tatizo la chronic alopecia, hali inayoweza kusababisha mtu kupoteza nywele akiwa katika umri mdogo, jambo ambalo limechangia baadhi ya watu kushangazwa na muonekano wake..jpg)
Kinachofanya simulizi la Yalcouyé livutie zaidi upande wa Tanzania ni kwamba kabla ya kuendelea na safari yake ya soka hadi Ulaya, alihusishwa na Simba SC. Taarifa zinaeleza kuwa mwaka 2022 Simba iliwahi kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili Yalcouyé alipokuwa ASEC Mimosas, lakini dili hilo halikukamilika. Inadaiwa ASEC ilikuwa imewataka Simba kulipa ada ya usajili ya takribani dola 250 pekee, lakini Simba ikaamua kutokamilisha uhamisho huo. Miaka kadhaa baadaye, Yalcouyé sasa anaonekana kwenye jukwaa kubwa la soka akiwa Brighton, jambo ambalo linazua swali la kama Simba ilipoteza moja ya fursa adimu ya kugundua kipaji mapema..jpg)
Kwa takwimu alizoonyesha dhidi ya Chelsea, Yalcouyé alionyesha kuwa si mchezaji wa kufunga tu bali pia ana uwezo mkubwa wa kushindana na wapinzani, kuwapita na kushiriki katika ujenzi wa mchezo. Alifanya touches 47 na recoveries mbili, huku bao lake likimpa umaarufu zaidi. Brighton tayari imejijengea sifa ya kugundua na kuendeleza vipaji, hivyo kama Yalcouyé ataendelea na kiwango hiki, si jambo la kushangaza kuona thamani yake ikipanda kwa kasi katika miaka ijayo. Kutoka kwenye akademi ya ASEC, kupita kwenye rada ya Simba, hadi kuangaza Premier League, safari ya kijana huyu bado ndiyo inaanza.



