Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Manqoba Mngqithi, amesema kikosi chake kinatarajia kukutana na mtihani mgumu katika mchezo wa kwanza wa CAF Champions League dhidi ya Gaborone United ya Botswana, utakaochezwa Jumamosi, Septemba 5, 2026, katika Uwanja wa Gaborone National Stadium.
Mngqithi amesema amepata siku chache za kujiandaa na kikosi chake licha ya kuwa na ratiba yenye michezo miwili ndani ya kipindi kifupi. Kocha huyo amemtaja mwenzake wa Gaborone United, Sean Connor, akisema amefanya kazi kubwa tangu alipoanza kuiongoza timu hiyo na ameweza kuijenga kuwa kikosi chenye ushindani.
Akizungumzia ubora wa wapinzani wao, Mngqithi amesema Gaborone United ni timu imara hasa katika eneo la ulinzi, huku ikiwa hairuhusu mabao mengi. Ameongeza kuwa timu hiyo pia inaweza kuwa hatari kupitia mashambulizi ya kushtukiza na mipira iliyokufa, hivyo Yanga inapaswa kuwa makini katika maeneo hayo.
Mngqithi pia amegusia kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji muhimu wa Gaborone United, akiwemo Mothusi Johnson na Mpho Kgwaswane, akisema bado hawezi kutabiri athari ya kutokuwepo kwao katika mchezo huo. Pamoja na hilo, amesema wapinzani wao bado wana wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kuleta madhara, akiwemo kipa mwenye uzoefu, washambuliaji wawili wazuri, kipa kutoka Namibia pamoja na beki wa kulia anayemuelezea kuwa na uwezo mkubwa.
Yanga itaanza safari yake ya CAF Champions League ikiwa na lengo la kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya mchezo wa marudiano. Mchezo wa Gaborone United dhidi ya Young Africans SC unatarajiwa kuanza saa 7:00PM kwa muda wa Botswana, sawa na saa 8:00PM kwa muda wa Tanzania, huku macho ya mashabiki wa Wananchi yakielekezwa Gaborone National Stadium.



