Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Septemba 3, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC Mechi Namba 017: Singida BS 1-2 Simba SC
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza ametozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la kushutumu na kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu kwenye moja ya chapisho la mtandaoni kinyume na kanuni ya 49:3 & 49:4 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari wa Klabu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 49:7 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari.
Afisa kutoka Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Pablo Almasi ametozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la kusambaza machapisho kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii (instagram) yaliyobeba maudhui ya kumkashifu mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu lakini pia kuikebehi teknolojia ya Football Video Support (FVS) kwenye mchezo kati ya Young Africans na Coastal Union kinyume na kanuni ya 49:4 & 49:5 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari wa Klabu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 49:7 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari.
Mechi Namba 031: Singida BS 4-2 Polisi Tanzania
Klabu ya Polisi Tanzania imetozwa faini ya Sh.10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la kumjumuisha mchezaji mmoja pekee kutoka timu yake ya vijana kwenye orodha ya wachezaji 21 kwa ajili ya mchezo kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:6(6.2) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 032: JKT Tanzania 2-1 Namungo FC
Klabu ya Namungo imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam kuelekea mchezo tajwa hapo juu Agosti 29, 2026.
Namungo iliwasili uwanjani saa 1:55 Usiku badala ya saa 1:30 Usiku jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kamati inazikumbusha timu zote kuzingatia kikamilifu kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo
Mechi Namba 033: Simba SC 2-0 Geita Gold
Klabu ya Geita Gold imepewa Onyo kali kwa kosa la maafisa wake kuchelewa kwa dakika 15 kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi na uratibu wa mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu ya Geita Gold imetozwa faini ya Sh.10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa wawili pekee kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi na uratibu wa mchezo kinyume na matakwa ya kanuni ya 17.29(2.1.1).
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 034: Kagera Sugar 0-2 Azam FC
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imefuta Adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji Gibril Sillah wa klabu ya Azam katika mchezo tajwa hapo juu, baada ya kujiridhisha kupitia picha jongeyo na taarifa ya wataalamu kuwa mchezaji huyo hakustahili adhabu hiyo.
Uamuzi huu ni kwa kuzingatia kanuni ya 12:8 ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Mwamuzi wa akiba wa mchezo tajwa hapo juu, Greyson Buchard kutoka Kagera amepewa Onyo Kali kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Klabu ya Azam imepewa Onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na Kocha Msaidizi kwenye Mkutano wa Wanahabari siku moja kabla ya mchezo kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:57 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 03: Singida BS 3-2 Namungo FC
Meneja Mashindano wa klabu ya Singida Black Stars Tabitha Kidawawa shauri lake limepelekwa kamati ya nidhamu ya TFF, Tabitha amekuwa na makosa ya kujirudia ya kimaadili kwenye michezo ya nyumbani ya Ligi Kuu ya NBC ya klabu yake.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:9 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa viongozi.
TAARIFA
Kamati imemfutia adhabu ya kufungiwa miezi 12 aliyekuwa Kocha Mkuu wa IAA John Zongwe, Kocha huyo aliwasilisha ombi la kupunguziwa adhabu hiyo akieleza mafunzo aliyoyapata baada ya adhabu hiyo na kuahidi kuwa balozi mzuri kwa Makocha wengine.
Zongwe alifungiwa kwa kipindi cha miezi 12 baada ya kubainika kumchezesha mchezaji ambaye katika mchakato wa usajili wake wa kujiunga na IAA alitumia jina la Joseph Ombeni (Jina sahihi), badala ya Bryson Urio ambalo ndilo linatambulika kwenye mfumo ili kukamilisha mchakato wake wa kujiunga na timu ya IAA jambo ambalo lilionekana kukiuka taratibu za usajili wa wachezaji.
Zongwe alikuwa tayari ametumikia miezi sita (6) ya adhabu yake, jambo ambalo pia limezingatiwa katika uamuzi wa kumruhusu kurejea kwenye shughuli za mpira wa miguu.



