Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kipo Malawi kikiwa na lengo la kuonyesha soka safi na kupata ushindi dhidi ya Mighty Wanderers katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo utakaopigwa kesho Jumapili katika Uwanja wa Bingu, Barker amesema wanafahamu ubora wa wapinzani wao, akibainisha kuwa Mighty Wanderers ina wachezaji wenye uzoefu, wakiwemo wanaowakilisha timu zao za Taifa.
Hata hivyo, kocha huyo amesisitiza kuwa Simba ipo tayari kwa changamoto hiyo na inalenga kupata matokeo chanya yatakayoiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwenda hatua inayofuata.
“Kila timu iliyoko kwenye michuano hii inataka kuvuka na kusonga mbele kama ilivyo kwetu Simba.”
“Mighty Wanderers ni timu nzuri inayoundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na wako katika timu zao za Taifa.”
“Lakini sisi tuko hapa kwa ajili ya kuonyesha soka safi na kupata matokeo chanya,” alisema Barker.
Simba yakamilisha maandalizi
Kikosi cha Simba kiliwasili Malawi jana na jioni kufanya mazoezi yake ya kwanza nchini humo ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo huo.
Leo, Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kufanya mazoezi yao ya mwisho katika Uwanja wa Bingu.
Simba inalenga kuondoka Malawi ikiwa na matokeo mazuri ili kujipa nafasi kubwa ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya juu ya klabu barani Afrika.