Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, amesema kikosi chake kinaendelea kuimarika na kuahidi kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, utakaochezwa Jumamosi.
Yanga imerejea nchini baada ya kutoka Botswana ambako ilicheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali dhidi ya Gaborone United na kutoka sare ya 1-1. Gaborone United ilitangulia kufunga kabla ya Selemani Mwalimu kuisawazishia Yanga katika dakika za nyongeza, akimalizia pasi ya Mudathir Yahya iliyoanzishwa na Maxi Nzengeli.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Mngqithi amesema anaamini timu yake itaendelea kuonyesha maendeleo na kupigania ushindi utakaoiwezesha kufuzu hatua inayofuata. Kocha huyo pia amesisitiza azma ya Yanga ya kupigania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, huku akiwataka mashabiki kuendelea kuiunga mkono timu katika safari hiyo ya kimataifa.