Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Shaban Kamwe, ametangaza kuwa mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Azam Complex utakuwa maalum kwa ajili ya kumuenzi mshambuliaji Selemani Mwalimu “Gomez”, kwa kuutaja kama “Sele Day.”
Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga watakaofika uwanjani kuonyesha upendo kwa nyota huyo kwa kuiga mtindo wake, hususan muonekano wa ndevu ambao umeanza kuhusishwa na Mwalimu tangu alipofunga bao la kusawazisha dhidi ya Gaborone United katika mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Botswana.
Hatua hiyo inalenga kuongeza hamasa na msisimko kuelekea mchezo huo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Yanga ikitafuta matokeo yatakayoisaidia kuvuka hatua ya awali baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.