Mchezaji wa zamani wa Manchester United na Juventus, Carlos Tévez, anapanga kufanya mchezo wake wa kuaga soka katika Uwanja wa La Bombonera, Argentina, mwezi Desemba 2026, miaka minne baada ya kutangaza kustaafu rasmi.
Katika mchezo huo, Tévez anatarajia kuwaalika baadhi ya mastaa aliowahi kucheza nao, huku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa miongoni mwa majina makubwa anayataka yashiriki katika tukio hilo. Tévez anataka kuwaona nyota hao wakicheza upande mmoja katika mchezo huo maalum.
Tévez amesema kuwa kuwaunganisha Messi na Ronaldo katika timu moja ni ndoto yake ya muda mrefu, akiamini tukio hilo litakuwa la kipekee kwa mashabiki wa soka duniani. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, nyota hao wawili tayari wamekubali kushiriki katika mchezo huo.
Tévez alicheza pamoja na Ronaldo akiwa Manchester United na Messi katika Timu ya Taifa ya Argentina. Pia aliitumikia Boca Juniors katika vipindi mbalimbali, akicheza jumla ya mechi 279 na kufunga mabao 94, huku La Bombonera ikiwa moja ya viwanja vyenye umuhimu mkubwa katika historia yake ya soka.