Wakala maarufu wa wachezaji, Jorge Mendes, amemtaja Lamine Yamal kuwa ndiye anayestahili kushinda tuzo ya Ballon d’Or 2026, akisisitiza kuwa nyota huyo wa Barcelona ndiye mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa. Kauli hiyo imekuja wakati mbio za kuwania tuzo hiyo zikizidi kushika kasi kuelekea hafla ya utoaji wa tuzo hiyo.
Mendes, ambaye ni wakala wa Yamal, alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Rais wa Barcelona, Joan Laporta. Akizungumza na waandishi wa habari, Mendes alisema: “Ballon d’Or ni kwa ajili ya Lamine Yamal, bila shaka yoyote,” huku akisisitiza kuwa kiwango cha Yamal kinamweka mbali na wagombea wengine. Kauli hiyo pia iliripotiwa na Goal baada ya kunukuliwa kupitia taarifa iliyosisitizwa na Fabrizio Romano.
Yamal mwenyewe amekuwa akionyesha kujiamini kuhusu nafasi yake katika mbio hizo, baada ya kuwa na msimu bora wa 2025/26 akiwa na Barcelona. Winga huyo alifunga mabao 24 na kutoa assists 18 katika mechi 45 za mashindano yote, huku Barcelona ikitwaa La Liga na Spanish Super Cup.
Kauli ya Mendes inaongeza nguvu katika mjadala wa Ballon d’Or 2026, ingawa Yamal anakabiliwa na ushindani kutoka kwa nyota wengine wakubwa akiwemo Kylian Mbappé na wachezaji wa Paris Saint-Germain. Kwa sasa, Yamal ni miongoni mwa majina yanayopewa nafasi kubwa katika kinyang’anyiro hicho.