Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema ushindi dhidi ya Azam FC ni muhimu kwa timu hiyo katika safari yake ya kuwania malengo ya msimu huu, huku akikiri kuwa maandalizi ya mchezo huo yamefanyika ndani ya muda mfupi.
Barker amesema Simba haikuwa na muda mrefu wa kujiandaa baada ya mchezo wao wa mwisho, lakini hilo halipunguzi umuhimu wa kupata matokeo mazuri dhidi ya Azam FC. “Tulikuwa na muda mchache wa maandalizi tangu kucheza mchezo wa mwisho, ila mechi hii ni muhimu kwetu kupata ushindi ili kufikia malengo yetu ya msimu huu,” alisema Barker.
Kocha huyo ameongeza kuwa Simba inalenga kubadilisha matokeo ya msimu uliopita dhidi ya Azam, ambapo ilipoteza jumla ya pointi nne katika michezo yao miwili ya Ligi Kuu. Barker amesema msimu huu wanataka kufanya vizuri zaidi katika michezo dhidi ya wapinzani wao hao.
Mchezo huo wa raundi ya sita ya NBC Premier League umepangwa kuzikutanisha Azam FC na Simba SC katika Uwanja wa Azam Complex. Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya kuanza msimu, huku Azam ikiwa miongoni mwa timu zinazoshindania nafasi za juu.