Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kesho, Septemba 17, 2026, kwa ziara inayolenga kukagua maendeleo ya maandalizi ya AFCON 2027.
Katika ziara hiyo, Motsepe ataungana na maofisa mbalimbali wa CAF kufanya ukaguzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, pamoja na kutathmini hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya mashindano hayo yatakayofanyika Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa TFF, Motsepe pia anatarajiwa kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya AFCON 2027, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, pamoja na viongozi wengine wanaohusika na maandalizi ya mashindano hayo.
Katika ziara yake, Rais huyo wa CAF atakagua maeneo mbalimbali ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kufuatilia maendeleo ya miundombinu na kuhakikisha maandalizi yanaendelea kwa kuzingatia mahitaji ya mashindano ya AFCON 2027.
Motsepe atakuwa ameambatana na viongozi kadhaa kutoka CAF na CECAFA, akiwemo Kurt Okraku, Feizal Sidat, Paulos Andemariam Weldehaimanot na Samson Adamu.
Ziara hiyo inatajwa kuwa sehemu muhimu ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Tanzania kuelekea AFCON 2027, huku nchi ikiwa miongoni mwa wenyeji wa mashindano hayo.