Baada ya kumaliza kazi yake dhidi ya Azam FC, Simba SC imegeuza rasmi nguvu zake kuelekea upande wa pili wa Jiji la Dar es Salaam, huku ikituma ujumbe mzito kwa Yanga SC kuelekea Dabi ya Kariakoo.
Kupitia chapisho lililowekwa na klabu hiyo, Simba imetumia picha yenye taswira ya staa wa filamu za mapigano Bolo Yeung akiwa amevalia jezi ya Simba, huku ikiambatanisha ujumbe mfupi lakini wenye uzito: “YOUR NEXT: YANGA.”
Ujumbe huo umeibua hisia kuelekea Dabi ya Kariakoo, ukionekana kuashiria kuwa baada ya Simba kumaliza majukumu yake dhidi ya Azam, Yanga ndiyo inayofuata kwenye orodha ya wapinzani wake.
Simba imeingia kwenye hali hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika Mzizima Derby, matokeo yaliyoongeza morali ndani ya kikosi na kuendeleza mwenendo wake mzuri kwenye mashindano ya ndani.
Sasa presha imehamia kwenye Dabi ya Kariakoo, mchezo ambao kila upande huingia ukiwa unatambua uzito wa historia, heshima na ushindani uliopo kati ya Simba na Yanga.
Kwa kutumia taswira ya Bolo Yeung, anayefahamika kwa nafasi zake katika filamu za mapigano, Simba imechagua lugha ya picha badala ya maneno mengi “Your Next: Yanga” ujumbe ambao umeweka wazi mpinzani anayefuata kwenye rada za Mnyama.
Kwa upande wa kikosi, ushindi dhidi ya Azam umeipa Simba nafasi ya kuendelea kujenga kujiamini kabla ya kukutana na Yanga.
Benchi la ufundi sasa linaelekeza nguvu katika maandalizi ya dabi hiyo, huku wachezaji wakitarajiwa kuingia kwenye mchezo wakiwa na morali iliyoongezeka baada ya kuvuka kikwazo cha Chamazi.
Dabi ya Kariakoo sasa imeanza mapema nje ya uwanja, huku mitandao ya kijamii ikiwa miongoni mwa maeneo ambayo Simba na Yanga hutumia kujenga hamasa kabla ya kukutana ndani ya uwanja.