Beki wa Geita Gold FC, Datius Peter, amesema tukio la kuchezewa rafu na kiungo wa Yanga SC, Stephane Aziz Ki, lilikuwa la bahati mbaya na si kitendo cha makusudi, huku akieleza kuwa anaendelea vizuri baada ya kupata maumivu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Septemba 15, 2026.
Datius aliumia baada ya Aziz Ki kumchezea faulo katika dakika za mwanzo za mchezo kati ya Geita Gold na Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex. Akizungumza baada ya mchezo huo, Datius alisema Aziz Ki hajawahi kuwa na rekodi ya kucheza madhambi ya aina hiyo, akiamini mguu wa kiungo huyo ulikuwa ukijaribu kukinga mpira.
“Aziz KI hajawahi kucheza rafu kama hizo, nafikiri ilikuwa bahati mbaya kwakuwa mguu wake ulitaka kukinga mpira sasa uwepesi wangu uwanjani ndio ikatokea hivyo,” alisema Datius, akieleza kuwa kwa sasa anaendelea vizuri na ameanza mazoezi.
Katika tukio hilo, mwamuzi Abdisalam Wajih alimwonyesha Aziz Ki kadi ya njano awali, kabla ya kwenda kwenye mfumo wa VAR na kubadilisha uamuzi huo kwa kumpa kadi nyekundu ya moja kwa moja. Yanga ilicheza ikiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 70, lakini ikafanikiwa kushinda 1-0 kupitia bao la Farouk Koumara.
Datius amesema baada ya tukio hilo alibainika kuwa na uvimbe katika eneo la enka na sehemu ya juu ya ugoko, lakini matibabu aliyopata yamesaidia hali yake kuimarika.