Kocha wa Namungo FC, Juma Mgunda, amesema ujenzi wa kikosi kipya unahitaji muda na subira, akieleza kuwa timu yake haikupata muda wa kutosha wa maandalizi ya msimu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara 2026/27.
Mgunda amesema mabadiliko ya kikosi na kuwasajili wachezaji wapya yanahitaji muda ili wachezaji wafahamiane, waelewe mfumo wa uchezaji na kujenga maelewano uwanjani. “Unapotengeneza timu mpya unahitaji muda na subira, kwa sababu mpira ni process, siyo kama unaweka chumvi kwenye mboga halafu ikakolea mara moja. Ni mchakato wa hatua kwa hatua,” amesema.
Kocha huyo amesema changamoto hiyo imeongezwa na ratiba ya msimu, baada ya ligi iliyopita kumalizika kwa kuchelewa huku msimu mpya ukianza mapema, hali iliyopunguza muda wa maandalizi ya pre-season. Kwa sasa, amesema Namungo inatumia kipindi cha mapumziko cha wiki tatu kama semi pre-season kurekebisha mapungufu na makosa yaliyoonekana katika michezo ya mwanzo.
Namungo imecheza mechi saba za ligi, ikishinda mbili na kupoteza tano, ikiwa na pointi sita na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo. Mgunda anatumia muda uliopo kuimarisha kikosi hicho kabla ya kurejea kwenye ushindani wa ligi.