Kiungo mshambuliaji wa Ghana, Mohammed Kudus, amejiondoa kwenye kikosi cha Black Stars kinachojiandaa na michezo ya kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Côte d’Ivoire na Gambia, licha ya awali kujumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 24 cha Kocha Carlos Queiroz.
Kudus amefanya uamuzi huo wakati akiendelea kurejea kwenye kiwango chake cha kimwili baada ya kukaa nje kwa takribani miezi saba kutokana na jeraha. Mchezaji huyo wa Tottenham Hotspur amerejea hivi karibuni kwenye soka la ushindani, akianza kujenga utimamu wake baada ya kipindi kirefu cha matibabu na urejeshaji wa mwili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa Ghana, Kudus anatarajiwa kubaki England na kuendelea na mchakato wake wa kurejesha utimamu wa mwili akiwa chini ya uangalizi wa Tottenham. Ghana Football Association tayari imepokea taarifa kuhusu uamuzi huo, huku hadi sasa ikiwa haijatangaza rasmi mchezaji wa kuchukua nafasi yake.
Black Stars itaanza kampeni yake ya kufuzu AFCON 2027 kwa kuikabili Côte d’Ivoire Septemba 24 mjini Bouaké, kabla ya kuikaribisha Gambia Septemba 29 katika Accra Sports Stadium. Ghana pia imepanga kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Morocco Oktoba 4.