Klabu ya Kagera Sugar imemteua rasmi kocha raia wa Burundi, Cedrick Kaze, kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo akichukua mikoba ya Juma Kaseja aliyetimuliwa kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya.
Kaze, ambaye anajulikana kwa soka la mbinu na uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuinoa Young Africans (Yanga) huko nyuma, anarehea nchini kukiokoa kikosi hicho cha 'Wana-Nkurukumbi' kilichopo katika hali mbaya.
Maamuzi ya uongozi wa Kagera Sugar kuvunja mkataba na Juma Kaseja pamoja na benchi lake lote la ufundi yamekuja baada ya timu hiyo kushindwa kupata ushindi hata mmoja katika michezo sita ya kwanza ya msimu wa 2026/2027.
Hadi sasa, Kagera Sugar imevuna pointi mbili tu kati ya 18 zinazowezekana, ikitoka sare michezo miwili na kupoteza minne, hali inayoiweka hatarini kwenye ukanda wa kushuka daraja.
Msemaji wa klabu hiyo amethibitisha kuwa makubaliano na Kaze yamekamilika na anatarajiwa kuanza kazi mara moja ili kukijenga upya kikosi hicho wakati huu ambao ligi imesimama kupisha kalenda ya FIFA.
Kibarua kikubwa cha kocha huyo mpya kitakuwa ni kurudisha morali ya wachezaji na kupata ushindi wa kwanza utakaofufua matumaini ya mashabiki wa mkoani Kagera.
Kaze amerejea nchini akitokea Afrika Kusini wiki chache baada ya kusitisha mkataba wake na Sekhukhune United inayoshiriki ligi kuu Afrika Kusini.