Msemaji wa Timu za Taifa Tanzania, Haji Manara, amesema kuna umuhimu wa kurejesha hamasa ya mashabiki viwanjani, akieleza kuwa kupungua kwa mwitikio wa watazamaji ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya timu, wasemaji na mashabiki.
Manara amesema kuelekea fainali za AFCON 2027, ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda, ni muhimu Watanzania kujitokeza kwa wingi kuziunga mkono timu za taifa pamoja na klabu zinazowakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Amesisitiza kuwa hamasa ya mashabiki ni sehemu muhimu ya mazingira ya mchezo, kwani viwanja vinapokuwa na watazamaji wengi huongeza hali ya msisimko na uungwaji mkono kwa wachezaji. Aidha, ameeleza kuwa wasemaji na wadau wa soka wana nafasi ya kuhamasisha jamii kuendelea kufuatilia na kuunga mkono timu za taifa.
Manara kwa sasa anaendelea na majukumu yake ya kuhamasisha michezo nchini, huku akishiriki katika shughuli mbalimbali za michezo na kuhimiza jamii kutumia michezo kama fursa ya kukuza vipaji na maendeleo.