Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali ya Tanzania imelipa Shilingi bilioni 104 katika maandalizi na upatikanaji wa haki ya matangazo kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, zitakazofanyika kwa pamoja Tanzania, Kenya na Uganda.
Makonda ameyasema hayo Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, Miss World na masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya sanaa. Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Kwa mujibu wa Makonda, Serikali inalenga kutumia AFCON 2027 kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, sambamba na kukuza sekta ya michezo, utalii na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na mashindano hayo.
Maandalizi ya Tanzania yanaendelea katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya michezo. Hotuba ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka wa fedha 2026/27 inaeleza kuwa ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ulikuwa umefikia asilimia 95, huku ujenzi wa uwanja mpya wa Arusha ukiwa umefikia asilimia 77.5 wakati wa taarifa hiyo.