Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amefikia makubaliano ya mkataba mpya wa muda mrefu na klabu hiyo, ambao unatarajiwa kumuweka Emirates Stadium hadi mwaka 2030. Taarifa hiyo imeripotiwa na mwandishi wa masuala ya uhamisho, Fabrizio Romano, huku hatua za mwisho za kukamilisha mkataba huo zikisubiriwa.
Kwa mujibu wa Romano, mkataba huo mpya utakuwa wa miaka minne na utaambatana na ongezeko la mshahara kwa Arteta. Pia, benchi lake la ufundi linatarajiwa kupewa mikataba mipya, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Arsenal kuendeleza mradi wake wa muda mrefu chini ya kocha huyo wa Kihispania.
Uamuzi huo umefuatia mafanikio makubwa ya Arteta msimu uliopita, ambapo aliiongoza Arsenal kutwaa taji la Premier League kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004, akimaliza kusubiri kwa miaka 22. Arsenal pia ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huo.
Arteta alichukua mikoba ya Arsenal Desemba 2019 baada ya kuondoka Manchester City, na tangu wakati huo amekuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya klabu hiyo. Endapo mkataba huo utakamilika hadi 2030, Arteta ataendelea kuiongoza Arsenal kwa zaidi ya muongo mmoja, huku klabu ikitarajia kuendeleza mafanikio yake ndani na nje ya England.