Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ujio wa kocha Steve Barker umeongeza kiwango cha kujiamini ndani ya kikosi hicho, hasa kuelekea michezo mikubwa kama Kariakoo Derby dhidi ya Yanga.
Ahmed amesema Barker tangu alipowasili Msimbazi hajawahi kuiona Simba kama timu inayopaswa kuwa mnyonge mbele ya mpinzani, akieleza kuwa kocha huyo ana kile alichokiita βkiburi cha kujiamini.β
Amesema hali hiyo si jambo jipya kwa Barker, akibainisha kuwa hata alipokuwa akiifundisha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, kocha huyo alikuwa na ujasiri wa kushindana dhidi ya Mamelodi Sundowns, moja ya klabu zenye mafanikio makubwa barani Afrika.
Kauli hiyo inakuja wakati Simba ikiendelea kujiandaa kwa Kariakoo Derby dhidi ya Yanga itakayochezwa Oktoba 10, 2026, huku timu zote zikiingia kwenye mchezo huo zikiwa zimeshinda michezo sita ya mwanzo ya Ligi Kuu.