Burudani ya soka la ndani inatarajiwa kushika kasi leo Ijumaa, Oktoba 9, 2026, pale viwanja vinne tofauti vitakapowaka moto kwa michezo minne ya Ligi Kuu ya NBC kuchezwa katika mikoa tofauti nchini.
Mzunguko huu wa nane unatarajiwa kushuhudia ushindani mkali huku kila timu ikisaka alama tatu muhimu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo inayozidi kuchanja mbuga.
Mzunguko wa leo utafunguliwa mapema saa 8:00 mchana pale Fountain Gate watakapowakaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Baadaye saa 10:15 jioni, jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City watakuwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine kupambana na Kagera Sugar, mchezo ambao unatazamwa kama mtihani mzito kwa timu zote mbili zinazohitaji kurekebisha makosa ya mechi zilizopita.
Saa 1:00 usiku, Dodoma Jiji watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri kuwabili Singida Black Stars, mchezo unaotabiriwa kuwa wa vuta ni kuvute kutokana na upinzani wa kikanda.
Pazia la burudani la leo litafungwa mkoani Tanga saa 3:00 usiku, ambapo Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' watamenyana na matajiri wa Chamazi, Azam FC, kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mchezo huu uliosogezwa mbele unatarajiwa kuvuta hisia za wengi huku Azam FC wakipania kupata matokeo mazuri ugenini baada ya kurejea kwa nyota wao waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa.
