Nyota wa Burundi, Saido Berahino, ametangaza rasmi kustaafu kucheza soka la ushindani baada ya kulitumikia kwa miaka 15, akisema anaondoka katika mchezo huo akiwa ametimiza mengi kutokana na fursa na manufaa aliyoyapata kupitia soka.
Berahino, ambaye aliwahi kucheza Ligi Kuu ya England (EPL) akiwa na West Bromwich Albion, amesema soka limempa kila kitu na kumwezesha kutoka katika mazingira magumu hadi kucheza katika baadhi ya ligi kubwa duniani. “Mpira wa miguu umenipa kila kitu. Kutoka mitaa ya Bujumbura hadi Hawthorns.
Kutoka Ligi Kuu England hadi katika maeneo ambayo sikudhani ningeweza kucheza. Mchezo huu umembeba mtoto mdogo mkimbizi katika maisha,” amesema Berahino.
Ameeleza pia shukrani zake kwa West Bromwich Albion kwa kumpa nafasi na kumuamini akiwa bado kijana.
“Napenda kuishukuru West Bromwich Albion kwa kuniamini wakati nilipokuwa mvulana. Miaka yote klabuni, mabao, mashabiki na nyakati, mara zote zitaendelea kuwa za kipekee. “Kwa kila mchezaji mwenzangu, kocha na shabiki ambaye ameshiriki katika safari, asante sana,” ameongeza.
Berahino ameelezea safari yake ya soka kuwa na changamoto pamoja na nyakati za furaha ambazo zimekuwa sehemu muhimu ya maisha yake ya kisoka.
Mshambuliaji huyo anatundika daruga akiwa na umri wa miaka 33, akiwa na uzoefu wa kucheza katika ligi za England na Ubelgiji.
Pia aliwahi kuziwakilisha timu za taifa za vijana za England katika viwango mbalimbali, kuanzia chini ya miaka 16 hadi chini ya miaka 21.