Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amekutana na kufanya kikao na viongozi wa klabu za Simba SC, Yanga SC, Azam FC na Singida Black Stars ambazo zimefuzu hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kikao hicho cha kimkakati kimefanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kikihusisha viongozi wa klabu hizo pamoja na viongozi wengine wa TFF.
Aidha, kikao hicho kimehudhuriwa na wasimamizi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni sehemu ya maandalizi na uratibu wa masuala yanayohusiana na michezo ya kimataifa.
Tanzania imefanikiwa kuingiza jumla ya timu nne katika hatua ya makundi ya michuano ya CAF msimu huu, hatua inayoongeza uwakilishi wa nchi katika soka la Afrika.
Kikao hicho kinakuja katika kipindi ambacho klabu hizo zinajiandaa na ushindani wa hatua ya makundi, huku mipango na uratibu mzuri vikitarajiwa kuwa muhimu katika kuhakikisha zinashiriki michuano hiyo kwa mafanikio.