Klabu ya Simba SC imepuliza rasmi kipyenga cha uchaguzi mkuu wa viongozi wake utakaofanyika Januari 3, 2027, huku zoezi la uchukuaji fomu kwa wanachama wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi likitarajiwa kuanza Oktoba 30, 2026.
Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa mchakato muhimu wa kisiasa ndani ya klabu hiyo yenye makazi yake Msimbazi, ambapo wanachama watapata nafasi ya kuwania uongozi na kuamua mwelekeo wa taasisi hiyo kwa kipindi kijacho.
Ratiba ya uchaguzi huo imetangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano, huku viongozi wa kamati hiyo wakieleza hatua zote zitakazofuatwa hadi siku ya kupiga kura.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Anderson Msumba, amesema lengo la kutangaza ratiba hiyo ni kuwafahamisha wanachama na wadau wa klabu kuhusu utaratibu mzima wa uchaguzi, kuanzia uchukuaji wa fomu hadi kutangazwa kwa matokeo.
Uchukuaji fomu kuanza Oktoba 30
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Alpha Gervas, wanachama wanaotaka kuwania nafasi za uongozi wataanza kuchukua fomu Oktoba 30 hadi Novemba 6, 2026.
Baada ya hapo, fomu hizo zitarejeshwa kuanzia Novemba 7 hadi 11, kabla ya kamati kuanza mchakato wa kuhakiki taarifa na vigezo vya wagombea.
Ratiba iliyotangazwa inaonyesha kuwa Novemba 12 hadi 14 itakuwa kipindi cha ukaguzi wa fomu, huku majina ya awali ya wagombea waliokidhi vigezo yakitarajiwa kutangazwa Novemba 15, 2026.
Hatua ya mapingamizi itafuata kuanzia Novemba 17 hadi 18, huku usikilizwaji wake ukipangwa kufanyika Novemba 23 hadi 25. Maamuzi kuhusu mapingamizi hayo yanatarajiwa kutolewa Novemba 26 hadi 27, kabla ya majina ya mwisho ya wagombea kutangazwa Novemba 30.
Kampeni kuanza Desemba 3
Baada ya kukamilika kwa taratibu za uhakiki na mapingamizi, wagombea watakaothibitishwa wataanza kampeni Desemba 3, 2026.
Kampeni hizo zitaendelea hadi Januari 2, 2027, siku moja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Januari 3.
Kipindi hicho kinatarajiwa kuwa muhimu kwa wagombea kueleza sera zao, mipango ya maendeleo ya klabu na namna wanavyokusudia kuimarisha Simba ndani na nje ya uwanja.
Wanachama watapata nafasi ya kutathmini ajenda za wagombea kabla ya kufanya uamuzi wao katika uchaguzi huo.
Nafasi saba za uongozi, mwanamke lazima apatikane
Katika maelezo yaliyotolewa na mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi, Richard Mwalibwa, nafasi saba za uongozi zimeainishwa, ambapo nafasi tano zitagombewa kupitia uchaguzi na nafasi mbili zitajazwa kwa uteuzi wa mwenyekiti atakayechaguliwa.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, nafasi ya mwenyekiti ina sharti la elimu ya shahada ya chuo kikuu, huku nafasi nyingine zikiwa na vigezo vya elimu vinavyotofautiana.
Aidha, katika nafasi tano zinazogombewa, angalau nafasi moja lazima ijazwe na mwanamke, hatua inayoweka wazi hitaji la uwakilishi wa wanawake katika uongozi wa klabu.
Mwalibwa ameeleza kuwa mgombea anatakiwa kuwa mwanachama wa Simba, kuwa na umri wa miaka 25 hadi 65 na kuwa amekamilisha angalau miaka mitatu tangu kupata kadi ya uanachama, pamoja na kutimiza masharti mengine yanayohusika na nafasi anayoomba.
Kwa nini Simba inafanya uchaguzi mwaka 2027?
Kamati ya Uchaguzi imeeleza kuwa mchakato huo unazingatia Katiba ya Simba ya mwaka 2018, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2025 na kusajiliwa Februari 2026.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Ibara ya 26 ya katiba ya klabu inaelekeza uchaguzi kufanyika kila baada ya miaka minne.
Msumba amesema uchaguzi uliopita ulifanyika Januari 2023, hivyo kipindi cha uongozi wa sasa kinaelekea ukomo wake Januari 2027.