Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema ana matumaini kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litatoa idhini kwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kutumika kuandaa mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya klabu barani Afrika msimu huu.
Akizungumza hii leo, Karia amesema TFF inaendelea na jitihada za kuhakikisha uwanja huo unakidhi vigezo vinavyotakiwa na CAF ili uweze kutumika katika michezo hiyo. Hata hivyo, idhini ya mwisho itategemea tathmini na uamuzi wa shirikisho hilo la soka barani Afrika.
Matumaini hayo yanakuja wakati klabu nne za Tanzania, Simba na Yanga zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na Azam FC na Singida Black Stars zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, zikiendelea na maandalizi ya kampeni zao za kimataifa. Endapo uwanja huo utaidhinishwa, klabu hizo zitapata fursa ya kuandaa mechi zao za nyumbani jijini Dar es Salaam.
Iwapo CAF itatoa idhini, hatua hiyo itakuwa nafuu kwa klabu husika pamoja na mashabiki wao, ambao watapata nafasi ya kushuhudia michezo hiyo jijini Dar es Salaam.