Klabu ya CD Tenerife imetangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha mshambuliaji wake Jesús de Miguel Alameda, kilichotokea Jumanne, Novemba 3, 2026, saa 8:00 asubuhi, kufuatia madhara makubwa aliyoyapata baada ya kugongana na kipa wa FC Andorra, Owono, katika mchezo wa timu hizo.
Tukio hilo lilitokea dakika za nyongeza za mchezo huo, ambapo De Miguel aligongana vikali na kipa huyo na kupoteza fahamu akiwa uwanjani. Taarifa zilizotolewa awali zilieleza kuwa mshambuliaji huyo alipata mshtuko wa moyo, hali iliyowalazimu wahudumu wa afya kumpa huduma ya ufufuaji wa moyo na kupumua (CPR).
Baada ya huduma hiyo, De Miguel alifanikiwa kurejeshewa mapigo ya moyo na kuanza kupumua mwenyewe, lakini aliendelea kuwa katika hali ya kupoteza fahamu na kupelekwa hospitalini kwa uangalizi zaidi. Mchezo huo ulisimamishwa ukiwa katika matokeo ya sare ya mabao 2-2.
Hata hivyo, CD Tenerife imethibitisha kuwa mchezaji huyo amefariki baada ya kushindwa kupona kutokana na madhara makubwa aliyoyapata katika tukio hilo.
Kupitia taarifa yake, klabu hiyo imeeleza kuwa imepokea habari hizo kwa majonzi makubwa, ikisema hakuna maneno yanayoweza kueleza maumivu waliyonayo wala kufuta huzuni iliyowakumba familia, marafiki, wachezaji wenzake na jamii nzima ya Tenerife.
Familia ya marehemu imewashukuru wote waliotoa pole na kuonesha upendo katika kipindi hiki kigumu, huku ikiomba kuheshimiwa kwa faragha yao wakati wa kuomboleza.