Kocha Mauricio Pochettino anatajwa kuwa chaguo linalopewa kipaumbele na Manchester United kuchukua nafasi ya Michael Carrick endapo klabu hiyo itaamua kuachana naye.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mkurugenzi Mtendaji Omar Berrada na Mkurugenzi wa Soka Jason Wilcox wamependekeza jina la Pochettino, huku viongozi hao wakitarajiwa kukutana Monaco leo kujadili suala hilo.
Pochettino anadaiwa kuwa na nia ya kujiunga na Manchester United, huku mazungumzo kuhusu masharti ya mkataba yakiendelea. Wakati huohuo, Carrick bado anasubiri taarifa rasmi kuhusu hatma yake na kwa sasa yupo katika uwanja wa mazoezi wa Carrington.
Hata hivyo, kumchukua Pochettino kutahitaji United kushughulikia kipengele cha kuvunja mkataba wake na Shirikisho la Soka la Marekani (US Soccer), kinachokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 10, huku gharama za benchi lake la ufundi zikiongeza takribani dola milioni 2.
Kwa sasa, Manchester United bado haijafanya mawasiliano rasmi na US Soccer kuhusu uwezekano wa kumchukua kocha huyo.
Chanzo: The Athletic.