Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeendelea kusaka ushindi wake wa kwanza katika michezo ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Nigeria, katika mchezo wa Kundi L uliochezwa nchini Nigeria.
Nigeria ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya pili kupitia Alhassan Yusuf, kabla ya Alphonce Msanga kuisawazishia Taifa Stars dakika ya 32 na kuifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili, Super Eagles walirejea kwa nguvu na kupata mabao mawili kupitia Tolu Arokodare dakika ya 52 na 60, na kufanya Nigeria kuondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania.
Matokeo hayo yanaifanya Taifa Stars kuendelea kukaa mkiani mwa Kundi L ikiwa na pointi moja baada ya michezo mitatu, huku Nigeria ikipanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi sita. Guinea-Bissau inaongoza kundi hilo kwa pointi saba, wakati Madagascar inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi moja baada ya michezo mitatu.