Kikosi cha Orlando Pirates kutoka Afrika Kusini kimetua jijini Dar es Salaam tayari kwa pambano kali dhidi ya wenyeji wao, Simba SC, katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Mchezo huo wa ufunguzi wa Kundi C unatarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 10:00 jioni, huku kila timu ikilenga kuanza hatua hiyo kwa ushindi.
Orlando Pirates, maarufu kama The Buccaneers, wamewasili nchini wakiwa na morali kubwa baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Golden Arrows siku ya Jumanne, matokeo yaliyowaimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (Betway Premiership).
Hata hivyo, wababe hao wa Afrika Kusini wamewasili bila kiungo wao tegemeo, Thapelo Mokobodi, ambaye alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Golden Arrows na anatarajiwa kukosa pambano hilo.
Kwa upande mwingine, Simba SC iliingia kambini tangu juzi kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mchezo huo muhimu, huku Wekundu wa Msimbazi wakilenga kutumia vyema faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao.
Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Steve Barker kimepania kuendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kama ilivyofanya katika ligi ya ndani.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kiwango kizuri kilichoonyeshwa na timu zote mbili katika mechi zao za hivi karibuni.
Simba itahitaji kutumia vyema uwanja wa nyumbani kuhakikisha inavuna pointi tatu muhimu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi ya klabu barani Afrika.