Uongozi wa klabu ya Al Ahly ya Misri umeanza kupanga mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho, kufuatia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Pyramids FC, ambapo bodi ya klabu hiyo imeidhinisha muundo mpya wa benchi la ufundi uliowasilishwa na kocha mkuu wa muda, Sami Komsan.
Mbali na mabadiliko ya benchi la ufundi, uongozi wa Al Ahly umeeleza kuwa uko tayari kusikiliza ofa kwa wachezaji ambao hawajafikia matarajio ya klabu.
Katika mpango huo, Al Ahly pia inalenga kuwapa nafasi zaidi vijana wenye vipaji ili kuthibitisha uwezo wao na kuwa sehemu ya dira mpya ya klabu. Mwelekeo huo unatajwa kuendana na matarajio ya kocha mkuu mpya au mkurugenzi mpya wa michezo kutoka nje ya Misri ambaye anatarajiwa kuteuliwa.
Hatua hizi zinafuatia taarifa ya klabu ya Novemba 24 iliyomshukuru Hussein Ammouta pamoja na wasaidizi wake, huku viongozi wa idara ya soka wakipewa jukumu la kuwasilisha majina ya makocha wanaoweza kuchukua nafasi hiyo. Komsan, ambaye sasa amepewa jukumu la kuiongoza timu kwa muda, aliwahi kushika nafasi hiyo mwaka 2022 baada ya kuondoka kwa Pitso Mosimane.