Nahodha wa Bayern Munich, Joshua Kimmich, amekosoa namna baadhi ya viongozi wa klabu hiyo walivyoshughulikia suala la afya na mkataba wa kiungo mshambuliaji Jamal Musiala, akisisitiza kuwa mijadala ya aina hiyo haikupaswa kupelekwa hadharani.
Kimmich ameeleza kuwa kauli za viongozi wakuu wa klabu hiyo, akiwemo Karl-Heinz Rummenigge na Uli Hoeneß, kuhusu uwezo na mkataba wa Musiala zimeibua mjadala usiofaa. Amesisitiza kuwa licha ya klabu kuwa na nafasi kubwa kuliko mchezaji mmoja mmoja, hilo halipaswi kuondoa umuhimu wa kuheshimu utu wa binadamu.
Kimmich anaamini kuwa masuala yanayohusu afya na mkataba wa Musiala yalipaswa kujadiliwa kwa faragha kati ya uongozi wa klabu na wawakilishi wa mchezaji huyo, badala ya kuyazungumzia kupitia vyombo vya habari. Kauli yake imekuja kufuatia maoni ya Hoeneß ya Novemba 8, ambapo alionyesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa Musiala kurejea katika kiwango chake cha awali, akigusia pia changamoto zake za kiafya na majeraha ya mara kwa mara.
Kimmich amesisitiza kuwa Musiala anaendelea kufanya kazi kwa bidii katika mazoezi na kwamba wachezaji wenzake wanamuunga mkono kikamilifu hadi atakaporejea katika kiwango chake.